Utangulizi
Wiki ya kuongeza uelewa kuhusu usugu wa vimelea kwa vijiuasumu (Antibiotics) duniani huadhimishwa mwezi Novemba kila mwaka. Madhumuni ya maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu usugu wa vimelea kwa vijiuasumu. Mwaka huu wafanyakazi na wanafunzi wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) watashiriki kuadhimisha siku hii kwa kutembea (Kuandamana) kutoka SUA hadi viwanja vya Sabasaba na kutoa ujumbe unaolenga unaoongeza uelewa wa jamii juu ya usugu wa vimelea kwa vijiuasumu.
Maadhimisho haya yatafanyika siku ya Jumamosi tarehe 14 Desemba 2019 kuanzia saa tatu asubuhi na kumaliza saa saba mchana katika viwanja vya sabasaba. Watu wote mmnaalikwa mjifunze namna ya kuepuka madhara yatokanayo na usugu wa vimelea kwa vijiuasumu. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050, watu milioni 10 kwa mwaka watakuwa wanakufa kwa sababu ya usugu wa vimelea kwa vijiuasumu. Ili kuepuka vifo hivyo kwa sasa elimu ya kutosha yafaa itolewe kwa jamii yote ili kuongeza uelewa kuhusu madhara yaletwayo na usugu wa vimelea kwa vijiuasumu.
Maana ya vijiuasumu
a) Ni dawa za kutibu magonjwa yanayosababishwa na vimelea kama vile bakteria
b) Dawa hizo hutumika kwa binadamu mfano: Amoxylin, Flagyl, PPF
c) Na kwa wanyama mfano: Teramycin (OTC), Penstrep
Maana ya usugu kwa antibiotiki
Ni hali ya vimelea vya magonjwa kutokufa kwa dawa iliyothibitika na inayotumika kuua vimelea hivyo
Sababu za usugu kwa antiobiotiki
a) Kutokumaliza dawa ulizoandikiwa na daktari
b) Kutumia dawa zisizo na ubora/feki
c) Kutumia dawa zilizoisha muda wake wa matumizi
d) Kula nyama, maziwa, mayai au damu yenye masalia ya antibiotiki kutoka kwa mifugo iliyotibiwa
e) Kutumia antibiotiki bila ushauri wa daktari
f) Utupaji holela wa mabaki ya dawa za antibiotiki
g) Kutumia dawa kwa namna isiyofaa mfano: kudunga dawa za kumeza
Madhara ya usugu kwa antibiotiki
a) Kutokupona ugonjwa hata baada ya kutumia antibiotiki ambazo zimekuwa zikitibu ugonjwa huo
b) Kuongezeka kwa gharama za matibabu kwa binadamu na wanyama
c) Kusambaa kwa vimelea vyenye usugu kwenye jamii ya binadamu na wanyama
d) Kupata magonjwa nyemelezi kutokana na tiba ya muda mrefu
Namna ya kuzuia usugu kwa antibiotiki
a) Kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalam wa tiba za binadamu na wanyama
b) Kuepuka kula nyama ambayo haijapimwa na mtaalam wa afya anayetambulika na serikali
c) Kuzingatia ushauri wa mtaalam kuhusu matumizi ya nyama, maziwa na mayai kutoka kwa mifugo iliyotibiwa na antibiotiki
d) Kutoazima dawa alizoandikiwa mtu mwingine
e) Kufukia mabaki ya antibiotiki kwenye shimo refu
f) Kusoma muda wa kuisha matumizi kwenye chupa/pakiti ya dawa
Ujumbe muhimu
a) Tumia dawa kwa usahihi. Jali afya yako!
b) Zuia usugu kwa antibiotiki, upunguze gharama za matibabu
c) Zuia usugu kwa antibiotiki kwa kuzingatia ushauri wa wataalam wa afya/mifugo
d) Kutumia dawa iliyoisha muda wa matumizi ni hatari kwa afya yako